Serikali yathibitisha Mzee Ngosha hakuwa mbunifu wa Nembo ya Taifa





Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura amesema kuwa marehemu Mzee Francis Kanyasu hakuwa mbunifu wa nembo ya taifa kama watu wanavyodhania bali alikuwa mchoraji.

Wambura amebainisha hayo leo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Devotha Minja alilouliza juu ya serikali kushindwa kumthaminipamoja na kumuhujumu Mzee Ngosha aliyechora nembo ya taifa na hatimaye kufa masikini.

"Si kweli kwamba Mzee Ngosha serikali imemuhujumu, kimsingi Mhe. Spika yapo majina mezani kama matatu hivi yanayohusiana na ubunifu wa nembo ambayo tunaitumia, nembo ya taifa. Kwa hiyo mpaka sasa bado haijajulikana nani hasa ambaye ni mbunifu wa nembo hii  kwa sababu mfano yupo marehemu ambaye alishatangulia mbele za haki muda mrefu ambaye anaitwa Abdallah Farhani wa Zanzibar yeye vielelezo tayari vishakutwa katika kumbukumbu zake jinsi alivyokuwa akibuni nembo yetu ya taifa, nembo ya Kenya pamoja na hata nembo ya OAU kipindi hicho alipokuwa anasoma Makerere University. Kwa hiyo yapo majina ambayo yanadaiwa kwamba yalishiriki katika kutengeneza nembo hii" alisema Wambura.

Pamoja na hayo Naibu Waziri amewaomba wataalamu kufuatilia kiundani kabisa juu ya suala hili ili waweze kutambua ukweli wake.