VIJIJI 15 WILAYANI HAI KUNUFAIKA NA MRADI WA VISIMA VYA UMWAGILIAJI


Kisima cha kisasa kwaajili ya shughuli ya kilimo cha umwagiliaji kilichopo  Kata ya Kia Kijiji cha Sanya Station,kilicho jengwa na Serikali kupitia bonde la Pangani chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 72 kwa saa.

HAI-Kilimanjaro


SERIKALI kupitia bonde la pangani imeanza kutengeneza visima katika vijiji 15 Wilayani Hai na kisima kimoja Kata ya Majengo wilayani Meru kwajili ya kilimo cha umwagiliaji .

Hayo yamebainishwa na Amiri Msangi toka Ofisi ya Bonde la Pangani wakati wa upitiaji na uandaaji wa katiba kwa vikundi vitakavyo faidika na mradi huo wa visima vya kisasa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo mchakato huo umeanzia kata ya Majengo Wilayani Meru.

Amesema kuwa lengo la mradi huo ni kumuwezesha mkulima kutumia na kujikita katika kilimo cha umwagiliaji  msimu wote wa kiangazi na masika  pasipo kutegemea mvua ambayo imekuwa haitabiriki kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Msangi amesema kuwa visima hivyo vitaweza kutoa maji kwa uhakika  ambapo kwa kila kisima kitakuwa na uwezo wa kutoa maji elfu Sabini na mbili kwa saa jambo ambalo litawezesha mkulima kufanya kilimo cha uhakika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa watumia maji Bonde la sanya kware Frank Kimaro amewataka wakulima hasa vijana kuwekeza katika kilimo hicho ili kuweza kupunguza tatizo la njaa na ukosefu wa ajira kwa vijana.

Ameongeza kuwa zaidi ya hekeri 300 zitakuwa na kilimo hicho cha umwagiliaji kwa uhakika ambapo uzalishaji utaongezeka kipindi chote cha mwaka,hali itakayo leta mapinduzi makubwa katika sekita ya kilimo.


Nyumba maalumu kwaajili ya kuweka mita na umeme utakao wezesha kisima kutoa maji na kurahisisha shughuli za kilimo.
Kwa upande wake Peter Lyimo Mjumbe katika kamati ya maji ya kijiji ameshukuru jitihada zilizo fanywa na serikali kupitia Bonde la pangani,kwa kuanzisha  mradi huo ambao utasaidia kupunguza makali ya maisha kupitia kilimo kama ilivyo kuwa hapo awali,kwa kutaka usimamizi wa mradi huo uwe endelevu katika maeneo mengi hasa yenye changamoto ya ukame.