NAIBU WAZIRI TAMISEMI:ATAKAYE SHAWISHI MWANAFUNZI KUPATA UJAUZITO KUKIONA CHA MOTO .

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mh.George Kakunda aliye simama akizungumza na Watumishi wa Halimashauri ya Wilaya ya Hai(kushoto) ni  Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Hai Onesmo Buswelu na (kulia) ni mjumbe toka TAMISEMI.



Hai-Kilimanjaro.



Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI George Joseph Kakunda amewataka Wazazi na Walezi Wilayani Hai  Mkoani Kilimanjaro kuacha tabia ya kufumbia macho watu wanaowapa ujauzito Watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka kumi na nane.

Kakunda ameyasema hayo alipo kuwa katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali iliyo fanywa kwa jitihada za wananchi na Serikali ikiwa ni pamoja na kuhamasisha juhudi za maendeleo ili kutekeleza sera ya Tanzania ya Viwanda.

Amesema kuwa hapo awali Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa ukisifika nchini kwa wazazi na walezi kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha Watoto wao wanakuwa wasomi, ila kwa sasa mambo ya mebadilika kwa baadhi ya wazazi na walezi kujihusisha na vitendo vya kuwapatia mimba watoto wa Kike walio chini ya umri wa miaka kumi na nane jambo ambalo limekuwa ni aibu kwa Mkoa.

“Serikali imejitahidi kubadilisha sheria kuanzia sheria ya elimu ya mwaka 1978 iliyo sema kuwa mtoto wa kike akipata mimba afukuzwe shule,adhabu ya mtoto wa kike peke yake huku aliye mpatia ujauzito akiachwa,Tumefanya mapitio makubwa mwaka 2002 Ya sheria ya elimu bado iliendelea kutoa adhabu kwa mtoto wa kike peke yake  tu.”alisema Kakunda.

Ameongeza kuwa sheria ya makosa ya kujamiiana iliyo tungwa mwaka 1998 ilitoa nafuu kidogo kwa mtoto wa kike kwa kutambua kuwa mtoto wa kike chini ya miaka 18 hata kama akipelekwa nyumba za wageni kwa dhumuni la kufanya mapenzi naye kwa kukubaliana au kuto kubaliana ni makosa ambapo kanuni ya adhabu ilifafanua vizuri adhabu inayostahili kutolewa.

Kakunda amesema kuwa mbali na sheria hizo kuwepo bado kuna watu wanacheza na sheria hiyo kwa kumpatia Mtoto wa kike ujauzito au kufanya ubakaji ila Mahakamani imekuwa ni tatizo kwa watu kuharibu ushahidi.

Akiongelea adhabu ya sheria ya mwaka 2016 marekebisho ya sheria ya elimu,serikali iliweka adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakaye msababishia mwanafunzi kupata ujauzito,au mtu aliye fanya njama kwa Mwanafunzi kuolewa lakini bado ushahidi unaharibika na kufanya sheria hiyo kutokufanya kazi inavyo paswa.

Katika hatua hiyo Waziri Kakunda amewataka viongozi wa kiserikali,dini na wananchi kukemea wahalifu hao ikiwa ni pamoja ya kuwafichua wahusika na kutoshawishika kuharibu ushahidi mahakamani ili haki iweze kutendeka.