Watoto wawili wafariki dunia kwa kula boga

WATOTO wawili wa familia moja, wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara, wamefariki dunia baada ya kula boga.

Wakati huo huo, watoto wengine watatu wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kula boga hilo linalodaiwa kuwa na sumu.


Waliopoteza maisha wametajwa kuwa ni Leiyoo Birikaa (6) na Nanyori Birikaa (12), wote wakazi wa Kijiji cha Partimbo, wakati waliolazwa hospitalini hapo ni Kitwaini Birikaa (12) Orkiang Birikaa (7) na Taleck Birikaa (6)

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Partimbo, Kimirey Mesiaya, aliliambia MTANZANIA jana kwamba aina ya boga lililosababisha madhara hayo, imekuwa ikitumiwa na wananchi wa kijiji hicho.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka Serikali ifanye uchunguzi wa maboga hayo kwa sababu yamekuwa yakiliwa na wananchi wengi kama sehemu ya vyakula vyao vya kawaida.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa madaktari wanaowatibu wagonjwa hao, Dk. Sarah Magoma, alithibitisha kupokewa kwa watoto hao na kusema walikuwa na matatizo katika maini kwa sababu yalikuwa hayafanyi kazi vizuri.

“Dalili za matatizo hayo ni kuumwa tumbo na kutapika, macho kubadilika rangi na kuwa ya njano na kutokwa damu puani na mdomoni.

“Pamoja na hayo, matatizo ya aina hiyo yamewahi kutokea wilayani Chemba na Kondoa. Kwa hiyo, tunaendelea kufuatilia chanzo chake kwa sababu watu wamekuwa wakipoteza maisha pamoja na jitihada zinazofanywa na madaktari,” alisema Dk. Magoma.