DC HAI NA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA HAI WAANZA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo,akimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Gasper Byakanwa (aliye kaa),kwa kuhamasisha ujenzi wa shule,katika kikao cha kusikiliza na kutatua kero za wananchi kata ya Bomang'ombe.

Wananchi wa Kata ya Bomang'ombe pamoja na wakuu wa idara wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Gelasius Gasper Byakanwa.

HAI-KILIMANJARO

WANANCHI walio telekeza na kushindwa kuendeleza  maeneo yao Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wamepewa muda wa siku 30 kuyaendeleza kabla Serikali haijabadilisha umiliki wa maeneo hayo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya yaa Hai Gelasius Gasper Byakanwa katika kikao na wananchi wa kata ya Bomang’ombe wakati akisikiliza kero za wananchi,ambapo aliongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Yohana Sintoo na wakuu wa idara walio kuwa wakijibu baadhi ya kero hizo.

Byakanwa amesema kuwa Mji wa Bomang’ombe umesha toka katika hadhi ya kijiji na kuwa mamlaka ya Mji,na kwamba Mji unakuwa na sifa zake ikiwa ni pamoja na utaratibu wa mpango mji,ambapo kwa sasa Mji wa Boma unatawaliwa na sheria zake.

“Sheria ya ardhi inatoa kipindi cha miaka 12 kushughulikia migogoro ya ardhi,ni vyema tukajua kuwa kila kitu kina ukomo wake,hivyo kwa wale wote walio na malalamiko yaliyo pitiliza miaka 12 wajue kuwa tayari malalamiko ya migogoro yao yamesha fungwa ”alisema Byakanwa.

Ameongeza kuwa serikali haita fumbia macho ukiukwaji huo huku ikifahamika kuwa watu hao wapo na wanafahamu wajibu wao wa kuyaendeleza.

“Wapo hadi viongozi wa serikali ambao wameshindwa kuyaendeleza maeneo yao akiwemo aliye wahi kuwa Mkuu wa wilaya ya Hai Jenerali Ulimwengu,hivyo sheria itafanya kazi yake kutengua umiliki huo baada ya siku 30 kumalizika”aliongeza Byakanwa.


Hata hivyo kero kubwa zilizo ibuka katika mkutano huo na kutafutiwa ufumbuzi  ni pamoja na migogoro ya ardhi,ukosefu wa mahali pa kuhifadhia taka pamoja na wafanyabiashara wa soko la walaji kulalamikia soko hilo kutokuwa na taa jambo linalopelekea vitendo vya wizi katika soko hilo nyakati za usiku.