MSONGO WA MAWAZO KWA WANAWAKE WANAO NYONYESHA NI TATIZO KWA MTOTO.





HAI-KILIMANJARO

Imebainika kuwa baadhi ya wanawake wanao jifungua wanashindwa kunyonyesha watoto wao ipasavyo kutokana na  kuwa na msongo wa mawazo  unao sababishwa na  akina Baba.

Hayo yamebainishwa na Dr Jane Mcharo  Mratibu wa Afya ya uzazi na Mtoto toka hosipitali ya Wilaya ya Hai alipo kuwa akizungumza na kituo hiki ofisini kwake kwa lengo la kujua umuhimu wa Wanaume wakati wa Mwanamke akinyonyesha.

Amesema kuwa Mwanaume ana mchango mkubwa sana kwa Mke wake hivyo kuhitajika kuhudhuria kliniki na Mke wake  kipindi cha ujauzito ili kuweza kupata elimu ya uzazi ya kumtunza mke na Mtoto.

Mcharo ameongeza kuwa wanaume wanahitajika kutumikia nafasi zao ipasavyo ikiwa ni pamoja na matunzo kwa Mama na Mtoto kwa kuwa nao karibu,huku akihakikisha kuwa mama na mtoto wanapaswa kula vizuri,kulala na kuvaa vizuri ikiwa ni moja ya nguzo muhimu ya jukumu lake.

Amebainisha kuwa Wanawake wamekuwa wakipata tatizo la kutokuweza kunyonyesha ipasavyo kutokana na msongo wa mawazo wanao pata toka kwa Mwanume ikiwa ni pamoja na baadhi ya Wanaume kutoka nje ya ndoa na kushindwa kutimiza majukumu yake ya kuleta chakula na mahitaji muhimu nyumbani.

Amesema kuwa ikiwa wanaume watatimiza jukumu lao inavyopaswa la kuhakikisha kuwa  familia yake inapata mahitaji muhimu kipindi cha uzazi wa Mwanamke kutasaidia kuondoa msongo wa mawazo kwa Mwanamke na kupelekea mwanamke kunyonyesha inavyo paswa kwa ustawi mzuri wa Mtoto na familia.