DC HAI:AWATAKA WAALIMU WA SEKONDARI WAJIPANGE KUIKIMBIA AIBU YA KUFELISHA .

Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa akizungumza na waalimu wa shule ya sekondari Kyuu katika ziara yake kwa shule zote za sekondari za Serikali.



HAI-KILIMANJARO.

Mkuu wa Wilaya ashangazwa na waalimu wa Shule za Sekondari Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro ambao baadhi yao hawajui nafasi za ufaulu katika shule wanazo fundisha jambo linaloashiria kiwango cha ufaulu kutokufikiwa kama inavyo hitajika.

Hayo yamebainika katika ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa  pamoja na Kaimu Afisa Elimu Sekondari Jafari Zaid  inayo endelea katika shule za sekondari za serikali kwa lengo la kutaka kujua mikakati waliyo jiwekea waalimu kuinua kiwango cha ufaulu.

Byakanwa ameshangazwa na waalimu wa shule hizo 17 alizo zitembelea baadhi yao wakiwemo waalimu wa Taaluma kutokutambua nafasi na kiwango cha ufaulu cha matokeo jambo linaloashiria kuwa waalimu hao hawana mpango wa kuinua kiwango cha ufaulu kinacho hitajika kwa wanafunzi wanao jiandaa na mitihani mwaka huu.

Amesema kuwa ni aibu kwa waalimu wa shule za sekondari wanaotegemewa kubadilisha matokeo na kuleta ushindani kwa shule zao kutokujua wanafanya vipi ushindani ilihali hawajui nafasi wanayo taka kuishindania kutokana na wao wenyewe kuto kujua nafasi yao ya ufaulu kiwilaya,Mkoa na Taifa.


Katika ziara hiyo inayo endelea kwa shule 29 za sekondari za serikali Byakanwa amewataka waalimu wakuu na waalimu wa taaluma kuweka mikakati ya pamoja na waaalimu wa idara za masomo yao ili kuweza kujinasua na aibu ya kufelisha  katika shule hizo ili waweze kuonesha wajibu na matunda ya kazi yao.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Sekondari Wilaya Jafari Zaid amewataka  wakuu wa Shule,waalimu wa taaaluma na waalimu wa idara za masomo kutimiza maelekezo yaliyo tolea  katika ziara hiyo ya mkuu Wa Wilaya kwa kuwasilisha mipango kazi yao katika ofisi ya Afisa Elimu Sekondari haraka na kuhakikisha kuwa wanabadilisha matokeo mabaya ya ufaulu kwa shule zao ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu kwa wanaofanya vizuri.