Mmoja wa Jamii ya Wafugaji Wilayani Hai akionesha shamba alilo andaa kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji. |
Hai-Kilimanjaro.
JAMII ya
wafugaji wa kabila la wamaasai Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wameanza
kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha mazao kwa wingi na kuepukana
na njaa kwenye familia zao.
Wakizungumza
katika kikao cha kupitia rasimu ya katiba ya vikundi vya umwagiliaji kwa
kutumia visima vya kisasa vilivyo chimbwa na serikali kupitia bonde la mto
pangani,wafugaji hao wamekiri kupokea mradi huo ili kuepuka kuwa omba omba wa
chakula kipindi cha kiangazi au panapo tokea uhaba wa chakula.
Kwa upande wake mmoja wa wafugaj hao Emanuel Laizer amebainisha
kuwa jamii hiyo ya wafugaji imekuwa ikiteseka kipindi cha kiangazi kwa kukosa
chakula katika familia zao kutokana na jamii hiyo ya wafugaji kuto kipa kilimo
kipaumbele katika jamii yao.
Ameongeza
kuwa ikiwa visima hivyo vitaanza kufanya kazi jamii hiyo itaweza kubadilisha
maisha katika kaya zao ikiwa ni pamoja na kulima kilimo cha biashara na kuweza
kujikimu katika ngazi ya familia.
Kwa upande
wake Amiri Msangi toka bonde la pangani ameelezwa kusikitishwa na kisima kilichopo
katika kijiji cha Sanya Station kata ya Kia
kuharibiwa miundombinu yake jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada
zinazo fanywa na Serikali kwa lengo la kusaidia wananchi wake.
Katika hatua
hiyo amewataka wananchi na viongozi walio chaguliwa kuwa walinzi wa mradi huo
kusudi mradi huo uweze kuwasaidia na kuwainua kiuchumi hasa wanawake na vijana
huku mradi huo ukipunguza tatizo la wafugaji kuhama na kutembea mwendo mrefu
kutafuta malisho kwa mifugo yao badala ya kuzalisha kupitia kilimo.