WAALIMU WA SEKONDARI TIMIZENI WAJIBU WENU KUINUA UFAULU WA MASOMO NA SHULE.

Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya Wavulana Lyamungo katika ziara yake ya kukutana na Waalimu wa Shule zote za Sekondari.
HAI-KILIMANJARO.

MKUU wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa Amewataka Walimu wa Shule za Sekondari Wilayani Hai kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kuinua kiwango cha somo na ufaulu katika shule wanazo fundisha, ili kutimiza haiba yao ya ualimu na kusaidia jamii kupata wasomi wenye faida.

Ameyasema hayo jana katika muendelezo wa ziara yake ya kutembelea shule za sekondari na kuzungumza na waalimu kwa lengo la kuwataka kuzinduka na kuanza ushindani wa kuonesha utekelezaji wa kazi waliyo somea.

Byakanwa amesema kuwa waalimu wanawajibu mkubwa wa kutumikia wanafunzi walio katika mikono yao ili kuweza kutengeneza viongozi na wataalamu wenye tija katika taifa ambao watapambana na elimu yao kwa kuliweka Taifa katika mikono salama kutokana na kufundishwa ipasavyo.

Aidha amepongea uongozi wa shule ya  Wavulana Lyamungo kwa kuweka utaratibu mzuri wa kumbukumbu ya wanafunzi walio fanya vizuri, ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia mpaka wanapo ingia kazini jambo ambalo litasaidia wanafunzi wengine kuweka bidii na ushindani katika masomo yao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa  Shule ya Wavulana Lyamungo Augustino Sanga amempongeza Byakanwa kwa utaratibu alioweka wakuzungumza na waalimu katika shule, jambo ambalo halikuwa likifanyika hivyo kuleta utengano baina ya wakuu wa Wilaya na Waalimu.


Hapo jana ziara ya mkuu wa Wilaya ya Hai ilifika katika shule ya wavulana Lyamungo,shule ya Lyasikika,Tumoni na Tumo ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo alipata nafasi ya kuzungumza na waalimu pamoja na wanafunzi,kwa lengo la kuwakumbusha wajibu wao katika utendaji wa kazi na masomo.