UFUNGUZI WA JUKWAA LA WANAWAKE LEO WILAYANI HAI (WANAWAKE WAKIUNGANA WANAWEZA).


Wanawake waliohudhuria ufunguzi wa Jukwaa la Wanawake kwaajili ya kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo Wilayani Hai Mkoani Kilimajaro katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.


HAI-KILIMANJARO.
IMEELEZWA kuwa kwa muda mrefu Wanawake wamekuwa hawapati fursa za kutosha za kiuchumi kutokana na kukosekana kwa usawa katika fursa,uwezo na kupata mitaji ajira na baadhi ya malipo ya kazi kwa wanawake yamekuwa siyo sawa na Wanaume.

Hayo yamebainishwa na Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jukwaa la Wanawake kwa ajili ya kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Edward Ntakiliho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hai ambapo Wanawake toka vikundi mbalimbali vya uwekezaji na ujasiriamali vilikutana.

Amesema kuwa ushiriki wa Wanawake katika vichocheo vya kiuchumi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla  kutokana na mwanamke kumudu kufanya kazi nyingi katika muda mchache ikilinganishwa na Mwanaume.

Ntakiliho ameongeza kuwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wa Wananchi kiuchumi limepewa dhamana ya kusimamia Sera na utekelezaji wa Eera ya Taifa kwa kuwaongoza Wananchi katika kufanikiwa kiuchumi kupitia Halmashauri za Wilaya na Taasisi nyingine.

Amesema kuwa Jukwaa la Wanawake litaweza kuongeza uelewa wa wanawake katika uchumi,biashara na upatikanaji wa mitaji na njia sahihi ya kutegemeana kiuchumi kwa halmashuri ya wilaya kuhakikisha kuwa inasimamia majukwaa ya kiuchumi katika kata na kufanya makutano kila baada ya miezi sita ndani ya wilaya.

Kwa upande wake Mratibu wa Jukwaa la Wanawake  Wilaya Frank Urio amesema kuwa jukwaa hilo litaweza kuwa kutanisha  wanawake katika biashara na ujasiriamali  wa bidhaa mbalimbalil ikiwemo ubunifu wa kuweza kumiliki viwanda kama sera ya Nchi inavyo elekeza.

Amesema kuwa Wanawake wamekuwa wakichangia pato la Familia mpaka pato la Taifa kwa utashi walio nao katika kuwekeza katika vikundi mbalimbali na kuweza kuji kwamua kiuchumi hivyo kuwa  nguzo muhimu ndani ya Familia na jamii.

Uzinduzi wa Jukwaa la Wanawake kwa ajili ya kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo ni Jukwaa lililo agizwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hasan kuelekeza Wilaya na Mikoa  kuunda na kuendesha majukwaa ya Wanawake kwa lengo la kuwa kutanisha na kujadiliana fursa,changamoto na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi ambapo Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro  imekuwa na kauli mbiu isemayo WANAWAKE WAKIUNGANA WANAWEZA.