HOSPITALI YA WILAYA YA HAI YAPOKEA MSAADA WA VITANDA 25 TOKA KWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI.


Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa wa kwanza kulia,akikabaidhi vitanda 20 magodoro na mashuka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hai Yohana Sintoo wa pili,pamoja na kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Bernadetha Swai.

HAI-KILIMANJARO

AHADI ya  serikali ya awamu ya tano ya kuboresha miundombinu na upatikanaji wa huduma za afya Kwa kila wilaya imetekelezwa kwa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro baada ya kukabidhiwa vifaa  vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 16.

Akizungumza katika zoezi la kukabidhi vifaa hivyo mkuu wa wilaya ya hiyo, Gellasius Byakanwa  alisema kuwa  vimetolewa  ili kuendeleza jitihada za serikali za kuimarisha huduma za afya nchini na ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais ya kuzipatia kila halmshauri vifaa hivyo.

Byakanwa alisema utoaji wa vifaa hivyo umekuja ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli ya kununua na kusambaza vitanda kwenye vituo vya umma vya kutolea huduma za afya nchini ambapo Wizara ya Afya ilitenga bilioni nne katika bajeti ya mwaka 2016/17, ili kuwezesha ununuzi na usambazaji wa vifaa vya hospitali katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Tunaishukuru serikali kwa kuipatia halmashauri  yetu , vitanda 20 vya kulaza wagonjwa,  vitanda vya kujifungulia 5, magodoro 20 na mashuka 20 vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 16,371, 100 alisema Byakanwa.

Naye Kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo, Denedicta Swai, alisema vifaa vitatumika kwenye vituo vya  kutolea huduma za afya  vya umma ambapo kwenye wilaya hiyo kuna vituo vya afya 4 , Zahanati 21 na  hospitali moja
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,  Yohana Sinto alisema vifaa hivyo walivyopokea vitasadia kuondoa uhaba wa vitanda ulikuwa unawakabili kwani jumla ya vitanda 120 vya kulazia wagonjwa  vilikuwa vikihitajika kulingana na idadi ya majengo yaliyopo na sasa .

“Tunaishukuru sana serikali imetusaidia sana kuondokana na upungufu wa vitanda kwa Halmashauri yetu  ilikuwa  na upungufu mkubwa lakini kwa sasa vitanda tulivyopatiwa vimesadia kupunguza idadi yake ambapo kwa sasa tunahitaji vitanda 100 pekee”alisema Sintoo.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema kuwa wanakabiliwa na upugufu wa watumishi wa afya zaidi ya 260 wa kada mbalimbali  na upungufu huu umeongezeka baada ya zoezi la uhakiki na kubaini zaidi ya watumishi wa afya kumi na tisa wana vyeti feki .

Moja ya ya vitanda pamoja na shuka zake vilivyo tolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa Hospitali ya Wilaya ya Hai.