Picha ikionesha muonekano wa Mlima Kilimanjaro katika kituo cha Shira cave mita 3750 toka usawa wa bahari. |
MOSHI.
IMEELEZWA kuwa
mabadiliko ya tabia nchi yameathiri viumbe hai pamoja na uchumi wa Taifa huku
wanyama pori wakiwa katika hatari ya kutoweka kutokana na uharibifu na shughuli
za kibinadamu.
Hayo yamebainishwa
na Kaimu mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Mtango Mtahiko wakati akifungua
warsha ya siku tatu ya uhifadhi kwa waandishi wa habari mkoa Kilimanjaro iliyo
fanyika Mjini Moshi.
Amesema
kuwa hifadhi 16 zilizopo chini ya TANAPA zina kabiliwa na changamoto
ya mabadiliko ya tabia nchi kutokana na athari zinazo tokana na shughuli za
kibinadamu ambazo siyo rafiki kwa mazingira kama vile uchomaji mkaa ndani ya
hifadhi,kilimo ndani ya hifadhi,ufugaji ndani ya hifadhi na
uharibifu wa vyanzo vya maji ndani ya hifadhi licha ya TANAPA kufanya jitihada
za kuondoa changamoto hizo kwa kutoa elimu kwa jamii zinazo zunguka maeneo ya
hifadhi.
Mtahiko amesema kuwa
Waandishi wa habari wanajukumu la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata na kupokea
habari muhimu za kutunza mazingira yanayo hifadhiwa ili kuweza kujenga kizazi
kitakacho yachukulia mazingira kuwa ni muhimu kwao na kuachana na uharibifu wa
mazingira yatakayo pelekea ukiwa kwa viumbe hai.
Ameongeza
kuwa hali ya Barafu katika kilele cha mlima Kilimanjaro
imezidi kupungua kutokana na changamoto alizozitaja hivyo kupelekea mabadiliko
ya tabia nchi kwa kupokea mvua kidogo,joto na maeneo mengine kukosa mvua
kabisa.
Naye Afisa uhusiano
toka TANAPA Pascal Shelutete amebainisha kuwa hifadhi ya mlima Kilimanjaro na
Hifadhi ya serengeti zimekuwa zikijiendesha zenyewe kwa kutoa gawio lake kwa
serikali tofauti na hifadhi nyingine duniani zinazo tegemea kupata ruzuku toka
serikalini,kutokana na usimamizi mzuri unao fanywa kuhakikisha kuwa sekta ya
uhifadhi inafanya kazi kwa faida .
Akizungumzia kuhusu
migogoro ya mipaka Shelutete amekiri kuwa kumekuwa na tatizo la migogoro ya
mipaka katika baadhi ya hifadhi na wananchi wanao zunguka hifadhi,ambapo tatizo
hilo linaweza kuvunja uhusiano mzuri uliopo kati ya shirika na wananchi,licha
ya jitihada mbalimbali kuchukuliwa na TANAPA kuondoa tatizo hilo.
Katika hatua hiyo
Shelutete amewataka wanahabari kutumia kalamu zao vizuri katika kutoa elimu kwa
wananchi,juu ya umuhimu wa kuhifadhi na kutembelea hifadhi za taifa kwaajili ya
kujifunza na kufurahia urithi huo wa asili,ili kujenga kizazi kitakacho
endeleza jitihada hizo za uhifadhi.
Warsha hiyo ya
Uhifadhi kwa waandishi wa habari ilifanyika kwa siku tatu mjini
Moshi ikiwa ni sambamba na wanahabari hao kutembelea kambi ya Shira Cave kuona
utalii wa uokoaji.