HAI-KILIMANJARO
Wazazi na walezi wameshuriwa kuwa karibu na watoto wao katika kipindi hiki wanapokuwa likizo za shule kufungwa ili kubaini changamoto mbalimbali zinzowakabili watoto pamoja na kuwaeleza madhara ya mimba za utotoni.
Akizungumza katika kipindi cha siku mpya kinachorushwa na Radio Boma Hai fm leo mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto wilayani Hai, Happyness Eliufoo alisema endapo wazazi watakuwa karibu na watoto wao katika kipindi hiki cha likizo itasaidia kupunguza tatizo la mimba pia watajua matatizo yanayowakabili watoto wao.
Eliufoo amesema kuwa tatizo la baadhi ya wazazi au walezi kushindwa kuwa karibu na watoto limechangia zaidi watoto kufanyiwa vitendo vya ukatali ikiwemo kupewa mimba kutokana na baadhi kushindwa kuwapatia elimu ya madhara ya mimba za utotoni.
Nae afisa kutoka shirika lisililo la kiserikali la Ajiso la Mjini Moshi ,Tatu Mruthu amesema kuwa ni vema wazazi au walezi wakatenga mda wa kukaa na watoto wao hali ambayo itasaidia kutambua na kujua changamoto wanazokabiliana nazo wawapo nyumbani tofauti na kipindi walipokuwa shuleni.
Kwa upande wake , afisa ustawi wa jamii kutoka wilaya ya Hai, Michael Mahundi licha ya wazazi kukosa mda wa kukaa na watoto wao bado jamii imekosa ushirikiano na kutoa taarifa za matukio mbali mbali ya ukatili wanaofanyiwa watoto nyumbani jambo ambalo limechangia kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukatli kwenye jamii.
Akichangia kwa njia ya simu katika kipindi hicho, mkazi wa mtaa wa Uzunguni Praygodi Muro alisema tatizo la mimba shuleni limechangiwa sana na umbali kutokana na baadhi ya watoto kutembea zaidi ya kilometea tatu kufuata shule ambapo wanafunzi huweza kukutana na vishawishi wakiwa njiani.