MKUU wa shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu St.Francis Of Assis Sister Costantina Mosha akichangia katika kikao hicho cha wadau wa elimu wilaya ya Hai |
HAI
WADAU wa
elimu wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kupitia wizara ya
elimu kuangalia na kuzifanyia kazi changamoto zinazo kabili wanafunzi,waalimu
na shule ili kuweza kuinua kiwango cha ufaulu hapa nchini.
Wameyasema hayo
walipokuwa katika kikao cha pamoja cha wadau wa elimu kwa lengo la kuangalia
mbinu mbali mbali zitakazo weza kutumika kuinua kiwango cha ufaulu katika shule
za wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto za wanafunzi wasiyo
jua kusoma na kuandika,mporomoko wa maadili pamoja na uhaba wa vitendea kazi na
mazingira ya kufundishia.
Awali
akifungua kikao hicho cha wadau wa elimu mwenyekiti wa wadau hao,Katibu Tawala
wa Wilaya Upendo Wela amewataka wadau kubuni njia itakayo saidia wanafunzi
kuweza kusoma,kuhesabu na kuandika maarufu kama K.K.K kabla ya kumaliza darasa
la saba ili kujenga Taifa la wasomi wenye uelewa.
“Nawaomba
wadau wote wa elimu kubuni njia mbadala zitakazo weza kutumika shuleni hasa
wilayani kwetu zitakazo tusaidi kuinua kiwango cha ufaulu ikiwa ni pamoja na
kuweza kubadilishana uzoefu pale inapo bidi, ili mwanafunzi aweze kupata elimu
iliyo bora hata kama atasindwa kufaulu basi aweze kumaliza darasa la saba akiwa
na uwezo wa kusoma,kuandika na kuhesabu”alisema Wela.
Kwa upande
wake Mwalimu mkuu wa shule ya wanafunzi wenye uhitaji maalumu St.Francis of Assis,Sister
Costantina Mosha amesema kuwa ni vema serikali kurudisha mfumo wa kurudia
darasa ili kuweza kuwachuja wanafunzi wasiyo jua kusoma,kuhesabu na kuandika
ambapo itasaidia kupata na kuondoa kabisa wanafunzi wanao ingia kidato cha
kwanza walio na matatizo hayo.
“Mbali na
wanafaunzi hao kurudia darasa,wazazi nao waweze kushirikiana na waalimu kwa
kushauriana ikiwa mwanafunzi atakuwa na matatizo hayo ya kuto kujua
kusoma,kuhesabu na kuandika kufanya kazi nyingine za mikono ili kuweza
kujiajiri,mfano,kufinyanga bidhaa mbali mbali za udongo,kuchonga na ufundi wa
mambo mbalimbali”alisema Mosha.
Naye John
Mambo Mwalimu wa shule ya sekondari Hai ameiomba serikali kupitia wizara yake
ya elimu kuweza kuondoa mfumo wa kujibu mitihani kwa kuchagua herufi kwani kwa
kufanya hivyo kumekuwa kukiwafanya wanafunzi kubahatisha kujibu na kujikuta
wamefaulu kwa njia hiyo.
“Wizara ya
elimu iliangalie hilo kwani unakuta mwanafunzi hajui kusoma wala kuandika
lakini anafaulu kwa kubahatisha herufi ya majibu,ningeshauri kuwa majibu yawe
ya kuandika,kutaja na kuelezea ili kuzia wanafunzi wasiyo jua kusoma wala
kuandika kuingia kidato cha kwanza.Alisema Mambo.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewahakikishia wadau hao wa
elimu kuwa changamoto na mapendekezo waliyo yatoa yataanza kufanyiwa kazi na
mengine yatafikishwa sehemu husika ili kuweza kuinua chachu ya elimu ndani ya
wilaya ili kuthamini michango hiyo ya wadau mbali mbali wa elimu.
“Nawaomba
wadau wa elimu msichoke kusaidia waalimu na wanafunzi pale inapohitajika
kufanya hivyo,kwani kwa kutoa misaada mbalimbali na ushauri itasaidia kupunguza
baadhi ya changamoto zinazo kabili sekta ya elimu hapa wilayani.”Alisema Sintoo