SERIKALI YAITAKA JAMII KUSHIRIKI MAENDELEO



 
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadick akipokea mchango wa bati kutoka kwa Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Kaskazini Salie Mlay. (Picha zote na Adrian Lyapembile)
Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa akizungumza kwenye hafla ya kupokea mchango wa bati za ujenzi wa vyumba vya madarasa kutoka benki ya NMB

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini Salie Mlay akizungumzia ushiriki wa benki yake kwenye shughuli za maendeleo wakati wa kukabidhi mchango wa bati kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadick wilayani Hai.



HAI - KILIMANJARO

Serikali imewataka wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo katika maeneo yao hasa ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kusoma na kuondoa msongamano wa wanafunzi madarasani.

Rai hii imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadick kwenye hafla fupi iliyofanyika Kitongoji cha Gezaulole Wilayani Hai kwa aili ya kupokea mabati mia mbili ishirini na tano yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tano yaliyotolewa na benki ya NMB kwa lengo la kuiunga mkono serikali katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye maeneo yao hata kama kwa sasa hawana watoto wanaosoma kwenye shule hizo kwani huduma ya elimu ni endelevu na inadumu kwa muda mrefu; hivyo asiye na mtoto leo atakuwa naye baada ya miaka kadhaa.

Akitoa shukrani zake kwa benki ya NMB, Sadick amewapongeza kwa uzalendo wanaoonesha kwa kuchangia maendeleo na kuwaomba wasichoke kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua ubora wa elimu na hatimaye kufikia lengo la kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati.

Akiongea kwenye hafla hiyo Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Salie Mlay amesema benki yao ina sera ya kushirikiana na serikali kwenye shughuli za maendeleo na kuahidi kuwa tayari kuchangia pale watakapohitajika.

“Sera yetu ni kuhakikisha serikali inayokuwa madarakani tunaisaidia kwa kila hali na mali iweze kufanya kazi zake na kutimiza malengo yake kwa wananchi ndio maana leo hii tumesimama mbele yenu kuwakabidhi mabati mia mbili ishirini na tano na tutaangalia namna ya kufanya zaidi ya hapo” alisema Mlay.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Gasper Byakanwa ametumia hafla hiyo kuwaasa watendaji wa ngazi ya kata na vijiji wakiwemo madiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuendelea kuhamasisha maendeleo kwenye maeneo yao pamoja na kusimamia utunzaji wa mali zinazopatikana kwa nguvu ya jamii.

Katika kuelekea kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani hatimaye kuboresha ufaulu wa wanafunzi; wilaya ya Hai mpaka sasa imefanikiwa kujenga vyumba arobaini vya madarasa mapya.