VIONGOZI WA DINI ZOTE WILAYANI HAI MKOANI KILIMANJARO WAKUNA VICHWA KULINUSURU ZIWA BOLOTI NA MAZINGIRA YAKE.




Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo wa kwanza (kushoto),Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Gasper Byakanwa(katikati) na Katibu Tawala Wilaya Upendo Wela aliye simama,wakati wa makubaliano ya kupanda miti na viongozi wa Dini zote.
Viongozi wa Dini ya Kikristo wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Hai akitoa ufafanuzi wa hali halisi ya uharibifu katika ziwa boloti.

Viongozi wa Dini ya Kiislam wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Hai akitoa ufafanuzi wa hali halisi ya uharibifu katika ziwa boloti.

Hai-Kilimanjaro

Viongozi wa dini zote Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Gasper Byakanwa wamefanya mapatano ya kupanda miti katika ziwa boloti ili kulinusuru na uharibifu ulio likumba ziwa hilo kwa kipindi kirefu.
Wakifanya mapatanao hayo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkuu wa Wilaya hiyo amesema kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuhakikisha  kuwa ziwa hilo linarudi katika hali yake ya zamani wakizingatia maandiko na mafundisho wanayo yatoa kwa waumini wao.
“Kwakweli viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa uumbaji ulioharibiwa na binadamu unarudishwa katika hali yake ili kuweza kutimiza wajibu na agizo la Mungu la kututaka binadamu tuchunge na kutunza bustani yake.”alisema Byakanwa.
Byakanwa amesema kuwa mwaka 1990 serikali ya Japani ikishirikiana na serikali ya Tanzania zilifanya utafiti kuhusiana na lower high maeneo ya sanya station na rundugai na lower rom,ambapo utafiti huo ulikuwa ukiangalia eneo la lower high kuweza kutumiwa kama sehemu ya kilimo na hilo liliwezekana isipokuwa maji yalikuwa ni tatizo hivyo, utafiti kuonesha kuwa maji yangeweza kupatikana katika ziwa boloti ila kwa sasa limeharibiwa vikali na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Ameongeza kuwa hifadhi ya ziwa boloti kwa vyanzo vyake vya maji lilikuwa na uwezo wa kumwagilia zaidi ya hekari 500 ila kwa sasa hakuna maji yanayo weza kumwagilia hata nusu heka jambo ambalo ni hatari kwa kizazi cha sasa na baadae,hivyo viongozi wa dini kutakiwa kusaidi kuhifadhi uumbaji wa Mungu kwa kuangalia njia za kulinusuru ziwa hilo.
Kwa upande wake Mchungaji Nixon Sifueli Kowero kutoka usharika wa mudio amesema kuwa wananchi wanapaswa kupewa amri na siyo ombi kuwataka wananchi kupanda miti katika maeneo yao ya wazi wanayo miliki,na mabalozi kupita na kuhakikisha upandaji huo wa miti kama wanavyo fanya wakati wa kuchangisha michango ya shule inayo endelea.

Tukiri kuwa sisi viongozi wa dini tumechangia uharibifu mkubwa kwa kujisahau kuwa kumbusha waumini wetu na sisi wenyewe majukumu ya kulinda na kutunza uumbaji wa Mungu,kwasasa ni dhahiri kuwa tumepoteza uhalisia wa mazingira yetu kwa uzembe,hivyo tuungane pamoja pasipo kujali dini  zetu kufufua upya mazingira yetu.”alisema Kowero.
Ameongeza kuwa kwa wananchi waliokwisha kufanya uharibifu katika ziwa boloti serikali isiwafumbie macho badala yake wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa waharibifu wa vyanzo vingine vya maji kama chemichemi zilizopo wilayani  Hai.
Naye Mhifadhi ujirani mwema kutoka KINAPA Hobokela Mwamjengwa amewataka viongozi hao wa dini kutenga sadaka zitakazo tumika kuchangi kufufua upya uumbaji Wa mungu ulilo haribiwa vibaya na binadamu ili kuweza kuepuka adhabu siku ya kiama.
Amesema kuwa ni vema viongozi wa dini kutenga utaratibu utakao wawezesha kushiriki vema katika kutunza mazingira yaliyo wazunguka na katika vyanzo vya maji vilivyo kuwa vikitumika zamani kutoa huduma ya maji ambapo kwa sasa vimeharibiwa ili kutimiza wajibu wao mbali na kufundisha masuala ya utoaji huku mazingira yakiteketea vibaya.
Katika Mkutano huo wa viongozi wa Dini na Mkuu huyo wa Wilaya walipatana utekelezaji huo kuanza mara moja ili kunusuru ziwa hilo,ambapo mwezi machi 9 mwaka huu zoezi hilo litaanza rasmi.
picha zote na Mwandishi wa Haikaziblog