DC:HAI, ATOA MIEZI MIWILI VYUMBA VYA MADARASA KUKAMILIKA.

Mkuu  wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa akimsisitiza  Diwani wa Kata ya Hai Mjini Joel Nkya(kushoto) kuhamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kumalizika kwa miezi miwili,kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Helga Mchomvu.
Hai-Kilimanjaro.

WANANCHI  na wadau wa elimu Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro,wametakiwa kujitolea katika kuandaa mazingira mazuri ya wanafunzi kupata elimu bora ili kuweza kuinua kiwango cha elimu.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa wakati akikabidhi mabati 54, yaliyo ahidiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadick katika ujenzi wa chumba kimoja kati ya  vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Geza ulole.

Amesema kuwa mbali na  Mkuu wa Mkoa kutimiza ahadi hiyo wapo wadau mbalimbali wamejitokeza kuunga mkono ujenzi wa vyumba vya madarasa ,ambapo wameguswa kufanya hivyo ili kuinua  kiwango cha ubora wa ufaulu na ufundishaji shuleni.

Katika kuunga mkono jitihada hizo Byakanwa ametimiza ahadi yake ya kuchangia mbao za kuezeka vyumba viwili vya madarasa kama alivyo ahidi katika shule hiyo,huku utaratibu mwingine ukilendelea katika shule zninazo lengwa kuongezewa vyumba na ukarabati wa madarasa.

“Niseme kuwa wananchi nao wanahitajika kuchangia shughuli hii,hivyo baadhi ya mambo mengine wanapaswa kushirikishwa na wao washiriki kikamilifu,nisinge penda kuona wala kusikia wananchi wanakwepa na kuwaachia kazi hii wadau na wafadhili”alisema Byakanwa.

Naye Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya hiyo Helga Mchomvu amepongeza na kuunga mkono utendaji kazi wa Mkuu wa wilaya hiyo.

“Nishukuru kwa kila jitihada nzuri zinazo fanywa za kuchochea maendeleo katika Wilaya yetu haswa kwa chahu hii inayo toka kwa Mkuu wetu wa Wilaya,tuahidi kuunga mkono jitihada hizi ili kuweza kuwapatia watoto wetu elimu iliyo bora”alisema Mchomvu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Geza ulole Simon Nyampanda amepongeza jitihada mbalimbali zinazo fanywa na Mkuu wa wilaya hiyo  katika kuboresha elimu pamoja na kuhamasisha shughuli za kimaendeleo pasipo kujali itikadi za vyama.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kukabidhi mabati 38 katika shule ya Msingi Hai pamoja na papi za kuezeka baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Uhuru.

Katika hatua hiyo, shule hizo zimepewa muda wa miezi miwili kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ili wanafunzi waweze kuvitumia na kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa baadhi ya madarasa.

Mkuu wa Wilaya akikabidhi mabati  54 yaliyo tolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadick katika kuezeka chumba kimoja cha darasa kati ya vyumba vitatu katika shule ya Msingi Geza ulole.

Mkuu  wa Wilaya ya Hai akikabidhi papi kwa wajumbe wa kamati ya ujenzi shule ya Msingi Gezaulole.

Muonekano wa vyumba vitatu vya madarasa vinavyo tarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili iliyo tolewa na Mkuu wa Wilaya.

 Picha zote  na Haikaziblog