Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Gasper Byakanwa akizungumza na Madaktari wa Hosipitali ya Wilaya, mara baada ya kupokea malalamiko ya utoaji huduma usiyo mzuri katika hosipitali hiyo. |
HAI-KILIMANJARO.
MKUU wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Gellasius Byakanwa , amesema hali ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika hospitali ya wilaya hiyo, hairidhishi kutokana na baadhi ya madaktari kuendelea kufanya kazi kwa mazoea huku wengine wakishindwa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa wakati
Pamoja na utoaji huduma usioridhisha pia ametoa onyo kwa wale wote watakaohatarisha maisha ya mgonjwa kwa kutompatia huduma kwa wakati ikiwemo kuwaweka rumande wakati hatua za kinidhamu ziendelea kuchukuliwa
Byakanwa alitoa kauli hiyo wakati akiongea na madaktari wa hospitali hiyo baada ya kufanya ziara ya kustukiza katika hospitali ya wilaya na kukutana wagonjwa wakiwa wamelazwa wodini kwa siku mbili huku hakuna huduma zozote walizopatia na hakuna daktari wa zamu aliyepita kutoa huduma kwa siku mbili.
Alisisitiza kuwa tabia za baadhi ya madaktari wamechangia sana serikali kuona kana kuwa halijali wananchi wake kwa kushindwa kuwahudumia wagonjwa ipasavyo na huku wakiendelea kusubiri mwisho wa mwezi kupata mishahara wasioitumikia.
Alisema hospitali hiyo inatoa huduma kiholela kwani hakuna taarifa za makabidhiano kati ya daktari mmoja kwenda kwa daktari mwingine hii inajidhirisha jinsi gani hakuna uongozi bora katika hospitali hiyo na hakuna kumbukumbu za wagonjwa ili waweze kuhumiwa na atakaye kuwa zamu
“Nilifanya ziara hapa hospitali Aprili 8 na tisa na hali niliyokuta sio nzuri kwa siku zote wagonjwa hawakutembelewa na daktari na ukiangalia hizo siku ni siku za kazi kawaida nadhani hospitali hii inashida katika uongozi ”
“ Kutokana na kutokuwepo kwa kumbukumbu mmeshindwa kwa muda wote kumtambua aliyetakiwa kuwa zamu kwa muda wote mpaka ilipofika Aprili 11 huu ni uzembe wa hali ya juu kwa mnahatarisha maisha ya watu”
''Wakati wa kufanya kazi kwa mazoea umepita na ninyi mnaofanya kazi kwa mazoea ndiyo mnao sababisha Wagonjwa wanaofika Hospitalini hapa kuwalalamikia kwa kukosa huduma''
“Sitawafumbia macho watumishi wazembe nitawachukulia hatua stahiki kwa yoyote atakayehatarisha maisha ya mgonjwa,
Amesema atawalinda na kuwatetea wale wote wanaofanya kazi zao kwa waledi, uadilifu na moyo wa kizalendo kwani wanarejesha heshima ya madaktari ndani ya jamii kwa kuepuka vitendo vinavyochangia kuendelea kulaumiwa na wananchi
Hata hivyo aliwatahadhirisha madaktari hao kuwa lolote litakalotokea kwa mgonjwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa ikiwemo kuwaweka rumande na hatua zingine zikifuata ili kurejesha nidhamu
“Mimi hapa ndio mwenyekiti wa kamati usalama wa wilaya, na usalama ni pamoja na usalama wa maisha ya mtu najua hamwezi kuzuia kifo ila nisikie mtu kafa kwa uzembe wa dakatari hali hiyo inanikera sana sasa endelea kucheza na maisha ya mtu hapo ndipo tutakutana mahakama kutafsiri sheria ”alisema Byakanwa
Akizungumza kwa niaba ya Madaktari hao, Khalfan Mwanga Daktari Msaidizi wa Macho,alikiri kutokufanya kazi kwa waledi hali ambayo imepelekea hata baadhi ya wananchi kukwepa kufikia katika hospitali hiyo kutokana na baadhi yao kushindwa kufanya kazi kwa maadili.
“Mheshimiwa tumetambua kuwa hapa tulipo ni pachafu, na kwa sasa tutachukua ufagioa na kufagia ili pawe pasafi kwa kuhakikisha kuwa huduma zinakuwa bora na kuepusha manung’uniko kwa jamii ”alisema