WAFUGAJI HAI WATAKIWA KUPIGA CHAPA MIFUGO YAO .

Afisa Mifugo Wilaya ya Hai Eliya Machange akitoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Mtakuja Kata ya Kia kuhusu umuhimu wa kupiga chapa Mifugo,zoezi litakalo anza hivi karibuni wilayani Hai.


Hai-Kilimanjaro.
Wafugaji Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kushiriki katika zoezi la kupiga chapa mifugo yao ili iweze kutambulika kirahisi na kuepuka wizi wa mifugo ulio kuwa ukifanywa hapo awali ikiwa ni pamoja na kutambua mifugo ilipo toka kirahisi.

Rai hiyo imetolewa na afisa mifugo wilaya ya Hai Eliya Machange alipo kuwa akizungumzia umuhimu wa zoezi hilo la kuweka chapa kwa mifugo katika mkutano wa kijiji cha Mtakuja kata ya Kia.

Machange amesema kuwa katika sensa ya mifugo iliyo pita katika kijiji hicho kimoja cha Mtakuja kata ya Kia kulikuwa na Ng’ombe takribani 9,742 ambao watatakiwa kupigwa chapa.

Amesema zoezi hilo lita fanyika kwa Nchi nzima kwa lengo la kutambua mifugo hiyo inatoka wilaya gani hivyo wafugaji wanatakiwa kuondoa wasiwasi juu ya zoezi hilo muhimu.

“Hili zoezi ni muhimu sana na kila mfugaji anatakiwa kushiriki ili kutambua mifugo yake,na zoezi hili haliwezi kuathiri biashara ya kuuza mifugo wala shughuli ya kuchunga mifugo hiyo.Kule Kenya mifugo yao imepigwa chapa na inatambulika kiurahisi,itafika siku minada yote itazuia kupokea mifugo isiyo kuwa na chapa ”alisema Machange.

Machange amesema kuwa kwa wale wafugaji walio peleka mifugo yao malisho ya mbali watatakiwa kurudisha mifugo hiyo kwajili ya zoezi la kupigwa chapa ambapo kwa kila ng’ombe mmoja ita gharimu shilingi miatano.


Amesema kuwa serikali inataka kuondoa tatizo la mifugo kudhurura maeneo mbalimbali ya nchi na nchi jirani ili kusaidia kutambua mifugo hiyo na kuirudisha maeneo husika ili kuepuka mifugo ya wafugaji kutaifishwa kizembe.